IQNA

Chuki dhidi ya Uislamu

Waziri nchini Kanada alaani shambulio la chuki dhidi ya Uislamu kwenye msikiti

14:05 - April 10, 2023
Habari ID: 3476842
TEHRAN (IQNA)- Waziri wa Biashara wa Kanada, Mary Ng amelaani shambulio la chuki dhidi ya Uislamu lililolenga msikiti mmoja eneo la Markham, Ontario wakati mtu mmoja alipovunjia heshima nakala ya Qur'ani Tukufu na kujaribu kuwashambulia waumini kwa gari.

"Nimefadhaishwa sana kusikia uhalifu wa chuki na tabia ya ubaguzi dhidi ya Jamii ya Kiislamu ya Markham. Kwa Waislamu wa Markham na Kanada, ninasimama nanyi," ameandika Ng kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Waziri wa Biashara wa Kanada amesema: "Wakati wa Ramadhani, misikiti ni mahali pa jamii na amani, na kila mtu anapaswa kujisikia salama katika sehemu yake ya ibada." 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jumuiya ya Kiislamu ya Markham (ISM), ambayo ni moja ya taasisi kongwe na kubwa zaidi za Kiislamu nchini  Kanada, siku ya Alhamisi mtu mmoja alifika eneo hilo akiwa na gari ambapo aliingia msikitini na kurarua nakala ya Quran Tukufu. Mbaguzi huyo aliyekuwa akitoa nara za ubaguzi na chuki dhidi ya Uislamu, alijaribu pia kuwagonga Waislamu waliokuwepo eneo hilo kwa gari lake.

Maelfu ya Waislamu huhudhuria kwenye Jumuiya ya Kiislamu ya Markham (ISM), na kituo hicho kimekuwa na shughuli nyingi zaidi kwa sababu ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Shambulio hilo limefanyika katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani, ambao unatambuliwa kuwa mwezi mtakatifu zaidi katika kalenda ya Kiislamu.

Kanada (Canada) ni mojawapo ya vituo vinavyoibuka kwa kasi vya chuki dhidi ya Uislamu (islamophobia) na uhalifu wa chuki kote ulimwenguni.

Utafiti mpya uliofanywa na Baraza la Kitaifa la Waislamu wa Kanada (NCCM) umeonyesha kuwa, hujuma za chuki dhidi ya Waislamu nchini humo ziliongezeka kwa asilimia 71 mwaka 2021.

Utafiti huo umebaini kuwa, visa vilivyosajiliwa vya kushambuliwa Waislamu kwa misingi ya dini yao iliongezeka kutoka 84 mwaka 2020, hadi 144 mwaka 2021.

Baraza la Kitaifa la Waislamu wa Kanada limesema Waislamu kadhaa waliuawa katika hujuma hizo, huku likitoa mfano wa tukio la kuuawa Waislamu wanne wa familia moja wenye asili ya Pakistan mnamo Juni mwaka 2020 mjini Ontario, baada ya mtu mwenye chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu kuwagonga na gari kwa makusudi.

3483126

captcha