IQNA

Jinai za Israel

Israel yadondosha mabomu msikitini Gaza na kuua waumini 50

12:09 - November 16, 2023
Habari ID: 3477900
TEHRAN (IQNA)- Takriban watu 50 wameuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa wakati ndege za kivita za utawala wa Israel zilipodondosha mabomu katika msikiti mmoja katika mtaa wa Sabra katikati mwa Ukanda wa Gaza huku utawala huo ukiendeleza mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina katika eneo hilo.

Shambulio hilo lilitekelezwa Jumatano jioni wakati wa sala ya jamaa ambapo msikiti huo ulikuwa umejaa waumini.

Mashambulio mengine ya Israel dhidi ya minara ya mawasiliano huko Khan Yunis kusini mwa Ukanda wa Gaza yamepelekea mtoto mmoja kuuawa.

Israel imewahimiza Wapalestina kuhama kutoka kaskazini mwa Gaza kuelekea kusini kwa ajili ya usalama wao, lakini Wapalestina wanasema utawala katili wa Israel unadondosha mabomu kila mahali na hakuna mahali popote salama kwa sasa.

Hadi sasa, Wapalestina wasiopungua 11,500, wakiwemo watoto 4,710 na wanawake 3,160, wameuawa, na wengine karibu 32,000 wamejeruhiwa tangu Oktoba 7, wakati utawala huo ulipoanzisha vita katika eneo la pwani lililozingirwa.

Pia siku ya Jumatano, mkuu wa Idara ya Mifupa katika  Hospitali ya al-Shifa, hospitali kubwa zaidi ya Gaza, ambayo ilivamiwa na wanajeshi wa Israel siku ya Jumatano, amesema mabuldoza na vifaru vya Israel vimevamia kituo hicho, na kubomoa sehemu za majengo yake.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Habari ya Utawala wa Palestina yenye makao yake Gaza, vikosi katili vya Israel vilifyatua risasi kiholela dhidi ya yeyote aliyejaribu kuondoka hospitalini, na hivyo kuibadilisha hospitali hiyo kuwa "kaburi."

Akizungumza na mtandao wa televisheni ya Al Jazeera ya Qatar, Khaled Abu Samra, mmoja wa madaktari wa hospitali hiyo, amesema hifadhi ya maji ya kituo hicho imepungua sana. Daktari huyo pia amekanusha madai kwamba jeshi la Israel limetoa msaada wa matibabu kwa kituo hicho.

Utawala wa Israel umedai kuwa hospitali hiyo ina "kamandi" ya harakati ya Hamas, madai ambayo yamekanushwa vikali na kundi hilo la kupigania ukombozi wa Palestina.

Hamas imeutaka Umoja wa Mataifa kuunda timu ya uchunguzi ili kukanusha madai ya Tel Aviv kuhusu hospitali hiyo.

3486038

Habari zinazohusiana
captcha