IQNA

Uislamu na Ukristo

Mtazamo wa Qur'ani Tukufu Kuhusu Nabii Isa (Yesu)

18:28 - December 25, 2023
Habari ID: 3478087
IQNA - Uislamu na Ukristo ni dini zenye mitazamo sawa kuhusu mambo kadhaa. Linapokuja suala la mtazamo wa dini hizi mbili kuhusu Nabii Isa (Amani ya Mwenyezi Mungu Iwe Juu Yake-AS-) imani zote mbili zinamtambua Iss kama mtu muhimu, lakini kuna hitilafu kuhusu maisha yake, utume na hatima yake.

Mtazamo wa Uislamu kuhusu Nabii Isa ni dhahiri katika Qur'ani Tukufu, ambapo jina lake linaonekana zaidi ya mara ishirini na tano.

Kama Ukristo, Uislamu unashikilia mama yake alikuwa ni Bikira Maryam (Maria), huku Qur'an Tukufu ikimtaja Nabii Isa kuwa ni Masihi.

Qur'an Tukufu, sawa na Injili ya Luka, inasimulia mazungumzo kati ya Malaika Jibril na Bikira Maryam, akitabiri kuzaliwa kwa Yesu.

“Na pale Malaika walipo sema: Ewe Maryamu! Hakika Mwenyezi Mungu anakubashiria (mwana) kwa neno litokalo kwake. Jina lake ni Masihi Isa mwana wa Maryam, mwenye hishima katika dunia na Akhera, na miongoni mwa walio karibishwa (kwa Mwenyezi Mungu). (Surah Al-Imran, aya ya 45)

Hata hivyo, tofauti kubwa inajitokeza katika simulizi ya Qur'ani Tukufu kuhusu kuzaliwa kwa Nabii Isa, ambapo Maryam anafafanuliwa kuwa alijifungua chini ya mtende badala ya horini, kama inavyoonyeshwa katika Agano Jipya.

Maryam, mama yake Nabii Isa, alichukua mimba kwa amri ya Mwenyezi Mungu, bila kuguswa na vifungo vya ndoa. Kufuatia kuzaliwa kwake, alitafuta kimbilio Misri, ambapo Issa aliishi kwa siri kwa miaka kumi na miwili kabla ya kuhamia Sham na kukaa katika jiji la Nazareti.

Kwa mujibu wa simulizi za Kiislamu, Nabii Isa aliteuliwa kiungu kuwa Mtume akiwa na umri wa miaka 30. Utume wake ulihusisha uenezaji wa Ukristo na wito kwa watu kumkumbatia Mungu, amani, urafiki, na udugu.

Jitihada hii nzuri ilileta upinzani kutoka kwa jamii ya Wayahudi, na kusababisha majaribio ya kumuua. Hata hivyo, Mwenyezu Mungu aliingilia kati, akimwokoa kupitia maombezi ya Malaika Jibril.

Tofauti za kimsingi zinajitokeza katika ufahamu wa kimsingi wa Isa kati ya Uislamu na Ukristo. Ingawa Wakristo wanamwona Nabii Isa kuwa Mwokozi na 'Mwana wa Mungu', Waislamu wanamwona kuwa nabii.

Mafundisho ya Kiislamu yanadai kwamba neno "Mwana wa Mungu" ni la sitiari, linaloashiria mmoja wa manabii waliochaguliwa na Mwenyezi Mungu.

Nabii Isa mwenyewe amenukuliwa katika Qur'ani Tukufu akisema, "(Mtoto) akasema: Hakika mimi ni mja wa Mwenyezi Mungu! Amenipa Kitabu na amenifanya Nabii." (Surah Maryam, aya ya 30)

Kuna mitazamo mbalimbali kuhusu hatima ya Nabii Isa. Kwa mujibu wa kumbukumbu za kihistoria, tafsiri huanzia kwenye kifo chake hadi kupaa kwake mbinguni kwa amri ya Mwenyezi Mungu.

Aliposambaza mialiko ya kuikubali dini ya Mwenyezi Mungu, Isa alikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa viongozi wakuu wa Kiyahudi na marabi. Kulingana na simulizi moja, jitihada iliyoratibiwa ilisababisha kukamatwa kwake kwa usaidizi wa mmoja wa masahaba wake. Baadaye, kufuatia kesi, alisulubishwa hadi kifo.

Maelezo tofauti ya tukio hili muhimu hujaza vitabu vya historia na maandishi ya kidini miongoni mwa Wayahudi na Wakristo. Imani za Kiyahudi zinadai kwamba Nabii Isa alikamatwa, kuhukumiwa, na kuteswa hadi kifo chake.

Kinyume chake, Wakristo wanashikilia kwamba alikamatwa, aliteswa, na kusulibiwa hadi kufa na kisha kufufuliwa kimuujiza baada ya siku tatu, akapaa mbinguni.

Qur'ani Tukufu, hata hivyo, inatoa mtazamo tofauti, ikisisitiza kwamba mtu aliyekamatwa alifanana na Isa. Katika simulizi hii, kisa cha utambulisho kimakosa kilisababisha kesi isiyofaa, kuteswa na kifo cha mtu mwingine.

"Na kwa kusema kwao: Sisi tumemuuwa Masihi Isa, mwana wa Maryam, Mtume wa Mwenyezi Mungu - nao hawakumuuwa wala hawakumsalibu, bali walifananishiwa tu. Na hakika walio khitalifiana katika haya wamo katika shaka nayo. Wao hawana ujuzi nayo wowote, ila ni kufuata dhana tu. Wala hawakumuuwa kwa yakini." (Surah An-Nisa, aya ya 157)

captcha