IQNA

Jinai za Israel

Viongozi wa Ulimwengu Walaani Utawala wa Israel kwa Mauaji ya Watafuta Misaada wa Gaza

9:34 - March 02, 2024
Habari ID: 3478438
IQNA-Viongozi wa dunia wameendelea kulaani kitendo cha wanajeshi wa Israel kuwaua Wapalestina 116 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 760 waliokuwa wakisubiri msaada wa chakula katika Ukanda wa Gaza uliozingirwa siku ya Alhamisi.

Wizara ya afya ya Palestina imelitaja tukio hilo kuwa "mauaji ya halaiki" na kusema ni jinai ya hivi punde zaidi ya Israel dhidi ya raia wa Gaza, ambao wamekuwa chini ya mashambulizi ya mauaji ya kimbari ya Israel na kuzingirwa tangu Oktoba.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Mao Ning amesema China "imeshtushwa" na "ilaani vikali" shambulio hilo, na kuutaka utawala wa Israel usitishe  mapigano mara moja. Pia alitoa wito wa kulindwa kwa usalama wa raia na kuwasilishwa kwa misaada ya kibinadamu huko Gaza.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alichapisha ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X na kudai kwamba alilaani vikali mauaji hayo.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell alidai kuwa "ameshtushwa" na habari za mauaji hayo na kusema vifo hivyo "havikubaliki kabisa". Pia alisisitiza udharura wa kusitishwa kwa mapigano na haja ya kufikiwa kwa misaada ya kibinadamu Gaza.

Nchi kadhaa za Kiarabu na Kiislamu zikiwemo Jamhurii ya Kiislamu ya Iran, Saudi Arabia, Kuwait, Umoja wa Falme za Kiarabu, Qatar na Uturuki nazo zimelaani shambulio hilo na kubainisha kuwa utawala unaokalia kwa mabavu umekuwa ukiwalenga raia wasio na silaha na kutojali damu ya Palestina.

Tamko la Iran

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema kuwa, jeraha la Gazah halitafutika katika kumbukumbu za watu huru.

Nassir Kan'ani amesema pia kuwa, aibu ya kuunga mkono na kunyamazia kimya mauaji ya umati na mauaji ya halaiki haitafutika katika mapaji ya nyuso ya wanaotoa madai uwongo ya haki za binadamu.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran ameandika katika mtandao wa kijamii wa "X" kuwa: Zaidi ya raia 100 wa Palestina waliokuwa wakisubiri kupokea misaada ya kibinadamu katika Mtaa wa Al-Rashid katika mji wa Gaza waliuawa shahidi na zaidi ya watu 800 walijeruhiwa kutokana na mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema kuwa, jinai hizi za Wazayuni maghasibu katu haziwezi kusahaulika.

Rais wa Colombia Gustavo Petro amelitaja shambulizi hilo kuwa ni "mauaji ya halaiki" na kusema kwamba limemkumbusha mauaji ya Holocaust. Alitangaza kuwa Colombia itasitisha ununuzi wote wa silaha kutoka kwa utawala huo ghasibu na kutoa wito kwa ulimwengu kumzuia waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

Ben-Gvir awapongeza wanajeshi wa Israel

Wakati huo huo Waziri wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel mwenye misimamo mikali ya chuki amewapongeza wanajeshi wa utawala huo walioua zaidi ya Wapalestina 100 waliokuwa wakisubiri misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza uliowekewa mzingiro.

Itamar Ben-Gvir, anayeongoza wizara eti ya usalama wa taifa ya Israel amesema: "lazima tuwaunge mkono kikamilifu wapiganaji wetu mashujaa wanaoendesha oparesheni huko Gaza, ambao walichukua hatua barabara dhidi ya genge la watu wa Gaza ambao walijaribu kuwadhuru".

Ben-Gvir, vilevile ametilia mkazo tena takwa lake la kuzuia kuingizwa misaada ya kibinadamu huko Gaza, akidai kuwa "inahatarisha" wanajeshi wa Israel.

3487382

Habari zinazohusiana
captcha