IQNA

Fikra za Kiislamu

Qur'ani Tukufu inapiga marufuku kuvunjia heshima matukufu ya wengine

17:52 - August 31, 2022
Habari ID: 3475712
TEHRAN (IQNA) - Kuna aya ndani ya Qur'an Tukufu inayosisitiza uharamu wa kuyatukana masanamu ya makafiri, na maoni ya wafasiri wa Qur'ani na wanafiqhi kuhusu aya hii na sababu ya kuharamishwa kwake ni ya kuvutia.

Akizungumza katika kongamano la hivi majuzi, Hujjatul Islam Mohammad Soroush Mahalati alielezea kuhusu hilo. Hapa kuna nukuu kutoka kwa hotuba yake:

Je, kuna kizuizi chochote katika suala la mbinu inayotumiwa kwa wale wanaotaka kuleta mageuzi na kurekebisha jamii? Angeweza kutumia njia gani na ni njia gani zinapaswa kuepukwa? Ninataja moja ya mambo ambayo yanapaswa kuepukwa: Haturuhusiwi kutumia matusi na lugha chafu hata kama lengo letu ni takatifu.

Kupambana na ukandamizaji na dhuluma ni wajibu, lakini jinsi tunavyofanya na lugha tunayotumia ni muhimu. Ndivyo hivyo hivyo katika kupigana na nguvu za kiburi. Hivi ndivyo Qur'ani Tukufu inavyosema kuhusu suala hili.

Aya ya 108 ya Sura Al-An’am inatueleza kwa uwazi tunalopaswa kufanya: “ Wala msiwatukane hao wanao waomba badala ya Mwenyezi Mungu, wasije na wao wakamtukana Mwenyezi Mungu kwa jeuri bila ya kujua. Namna hivyo tumewapambia kila umma vitendo vyao. Kisha marejeo yao yatakuwa kwa Mola wao Mlezi, naye atawaambia waliyo kuwa wakiyatenda. "

Aya hii ina sehemu tatu. Sehemu ya kwanza inatanguliza marufuku. Pili ni uchambuzi wa kijamii na tatu ni uchambuzi wa kisaikolojia. Sijaona mtindo huu katika aya zingine zozote. Sehemu ya kwanza inaamuru kwa uwazi kutotumia lugha mbaya dhidi ya wasiokuwa Waislamu. Sababu ni nini? Sababu inakuja katika sehemu ya pili, inayosema ukifanya hivyo, wasiokuwa Waislamu wanaweza kufanya vivyo hivyo dhidi ya matukufu yako. Mnatukana sanamu zao na wanamtukana Mwenyezi Mungu wenu. Sehemu ya tatu inasema kila taifa lina usikivu juu ya imani na fikra zao hivyo huwezi kuwatukana na kutarajia hakuna majibu.

Aya hii iko wazi kabisa na dhana zake hazina utata. Tukizingatia hilo, kutakuwa na mabadiliko katika tabia na mwenendo wetu kama Waislamu. Haijalishi una lengo gani, unapaswa kutii sheria hii.

Aidha, aya hii na kanuni ni ya milele si ya muda.

Jambo lingine la kuzingatia hapa ni kwamba tunapaswa kuwa waangalifu sio tu juu ya maneno yetu lakini pia kuhusu tabia zetu tunaposhughulika na wasiokuwa Waislamu kwa sababu tabia zetu zinaweza pia kuvutia upande wa pili.

captcha