IQNA

Fikra za Kiislamu

Qur’ani Tukufu inawahimiza wanaadamu Kutafakari

22:59 - September 03, 2022
Habari ID: 3475728
TEHRAN (IQNA) – Katika aya nyingi za Qur’ani Tukufu, wanadamu wameshauriwa kutafakari ambapo aya zake nyingi zinasisitiza mantiki na fikra.

Wanafalsafa wanasema dini na falsafa zinaenda sambamba, au kwa maneno mengine Qur’ani na falsafa hazipingani.

Aya nyingi za Qur’ani Tukufu zinataka mwanadamu  atafakari na zinasisitiza kuhusu hekima na busara.

Aya ya 125 ya Surat An-Nahl inasema: “ Waite waelekee kwenye Njia ya Mola wako Mlezi kwa hekima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora. Hakika Mola wako Mlezi ndiye anaye mjua zaidi aliye ipotea Njia yake, na Yeye ndiye anaye wajua zaidi walio ongoka.”

Lengo la kuhimiza kutafakari na busara ni kuwaongoza wanadamu kwenye ukweli kwamba Mwenyezi Mungu yupo na mwanadamu anaweza kufikia wokovu na njia ya kuufikia ni kumwamini Mwenyezi Mungu na kumtegemea Yeye.

Sio tu kwamba Qur’ani inahimiza kutafakari, bali pia lugha ni moja ya mantiki na busara katika aya nyingi, ambazo baadhi zinathibitisha jambo fulani na nyingine zinapinga jambo fulani.

Katika Aya ya 22 ya Surah Al-Anbiya, kwa mfano, Mwenyezi Mungu anasema: “au wangeli kuwamo humo miungu wengine isipo kuwa Mwenyezi Mungu basi bila ya shaka hizo mbingu na ardhi zingeli fisidika. Subahana 'Llah Ametakasika Mwenyezi Mungu, Bwana wa A'rshi (Kiti cha Enzi), na hayo wanayo yazua.”

Aya hii inatoa hoja inayoegemezwa kwenye ulinganisho ambao kimantiki unathibitisha kwamba hakuna mungu mwingine ila Mungu.

Mfano mwingine ni Qur’ani inavyosema kuhusu ufufuo wa kimwili: “Na akatupigia mfano, na akasahau kuumbwa kwake, akasema: Ni nani huyo atakaye ihuisha mifupa nayo imekwisha mung'unyika?’” ( Surah Ya-Seen, Aya ya 78 ) Hii pia ni hoja ya kifalsafa.

Pia kuna mifano mingi katika Qur’ani katika suala la wito wa kufikiri kwa makini. Kwa mfano, ili kujua ukweli, Qur’anni inawataka watu wajifikirie wao wenyewe badala ya kuwaiga wengine kwa upofu: “ Na wanapo ambiwa: Fuateni aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu; wao husema: Bali tutafuata tuliyo wakuta nayo baba zetu. Je, hata ikiwa baba zao walikuwa hawaelewi kitu, wala hawakuongoka? “ (Surah Al-Baqarah, Aya ya 170)

Au katika Aya ya 36 ya Surah Al-Isra, Mwenyezi Mungu anasema: “Wala usiyafuate usiyo na ujuzi nayo. Hakika masikio, na macho, na moyo - hivyo vyote vitasailiwa.” Kwa hivyo mtu asichukue njia asiyoijua, au kumfuata mtu ambaye hamjui vizuri. Haya ni masuala muhimu sana katika fikra makini na kuna mapendekezo mengi kama hayo yanayohusiana na fikra makini katika Qur’ani.

captcha