IQNA

Matembezi ya Arbaeen

Matembezi ya Arbaeen yanakuza Umoja kati ya Waislamu, Ubinadamu

20:32 - September 15, 2022
Habari ID: 3475787
TEHRAN (IQNA) – Mamilioni ya Waislamu wako katika safari ya kuelekea kwenye haram tukufu ya Imam Hussein (AS), ili kuonyesha mapenzi na kujitolea kwao kwa mjukuu kipenzi wa Mtume Muhammad (SAW).

Safari ya Arbaeen, pia inajulikana kama matembezi ya Arbaeen, ndiyo inayowaleta wanaume na wanawake, vijana na wazee kutoka tabaka zote za maisha pamoja katika mjumuiko huu adhimu hadi sehemu alimozikwa Imam Hussein AS,  Imam wa tatu wa madhehebu ya Shia.

Lakini ni nini huwafanya watu watekeleze bila kuchoka safari hii ndefu na ngumu ambayo huchukua siku kadhaa na hata wiki kadhaa kila mwaka?

Utangulizi mfupi wa Arbaeen

Arbaeen ni neno la Kiarabu ambalo mane yake ni 40.  Katika muktadha huu, ni siku ya 40 tangu maadhimisho ya kuuawa shahidi Imam Hussein (AS) na masahaba wake watiifu tarehe 10 Muharram katika siku ya Ashura. Mtukufu huyo aliuawa shahidi katika mapambano ya Karbala  karne 14 zilizopita.

Siku ya Imam Hussein (AS) ya Arbaeen inakuja tarehe 20 Safar, mwezi wa pili wa kalenda ya mwandamo wa Kiislamu na mwaka huu inasadifiana na 17 Septemba.

Baada ya kufa shahidi Imam Hussein (AS) mikononi mwa katili Yazid bin Muawiya, watu ambao walishangazwa na ukatili wa ukoo wa Ummaya walianza kuzuru kaburi lake kutoa heshima zao.

Kizazi cha Imam Hussein (AS) pia kiliiweka hai mila hiyo kwa kuwahimiza watu kuzuru kaburi la Imam Hussein (AS), na hivyo ndivyo mila hiyo imeendelea hadi leo huku wanaozuru kaburi hilo takatifu wakiongozeka kwa mamilioni kila mwaka.

Hivi sasa, kaburi la Imam Hussein (AS) ambalo limepanuliwa na kufanyiwa ukarabati linaweza kuchukua idadi inayoongezeka ya wageni.

Tawala za kale kama vile za Bani Ummaya na Bani Abbas , na vile vile tawala za zama hizi kama utawala dhalimu Saddam Hussein na makundi ya kigaidi kama Daesh, zilipinga matembezi hayo na katika baadhi ya matukio yalipiga marufuku na hata kutishia kubomoa Haram Takatifu ya Imam Hussein (AS).

Walakini pamoja na kuwepo njama zote hizo, mila hii ya kale na ya kimaanawi imedumu kwa karne nyingi na sasa haiwezi kukandamizwa tena.

Kufanya matembezi kwa kawaida wafanyaziara hufika hadi Najaf kwa ndege au gari. Mji wa najaf ni sehemu alimozikwa Imam Ali ibn Abi Talib AS (baba yake Imam Hussein). Wafanyaziara hutembea kutoka Najaf hadi Karbala. Matembezi haya yatachukua kati ya siku tatu hadi saba.

Wafanyaziara wa Arbaeen wanakula na kulala wapi?

Ili kuwapa wafanyaziara chakula, mahali pa kupumzika, kuoga, nk misaada na watu wa kujitolea huweka makao yanayojulikana kama moukeb kando ya barabara ya kuelekea mji mtakatifu wa Karbala.

A boy offers drinks to pilgrims attending Arbaeen walk in September 2022.

Moukeb hizi hutoa huduma mbalimbali kama vile mahali pa kula, kulala, kupumzika, kuoga, na dawa na mengine mengi. Huduma zote ni bure na zinafadhiliwa na michango ya wafadhili.

Mbali na moukeb kuna vituo na stendi ambazo hutoa chakula na vinywaji bure. Hii ina maana kwamba wafanyaziara wanaweza kutembea hadi Karbala bila ya kuwa na wasiwasi kuhusu mahitaji yao ya kimsingi.

Arbaeen; Fursa ya kujitafakari

Wafanyaziara walioanza safari hii wanastahimili hali mbaya ya hewa ambapo katika miaka ya hivi karibuni Safar imeangukia katika msimu wa joto kali. Hali hii ngumu ya wafanyaziara huku wakiwa mbali na starehe za nyumbani inawakumbusha matatizo ambayo Imam Hussein (AS) na familia yake na masahaba walilazimika kuyavumilia siku ya vita vya Karbala.

Hali ngumu kama hizo huwasaidia watu kuwa na subira. Wakati wa kutembea, watu wana nafasi ya kujitafakari na kujichunguza.

Tofauti zikiwemo za rangi za watu, dini na kabila zinawekwa kando na wote hujumuika  pamoja katika kanuni kukataza maovu na kuamrisha mema.

Watu wanaoshiriki husimulia yaliyojiri katika safari na husisitiza jinsi matembezi hayo yanavyokuwa na mvuto wa aina yake ambao humfanya mshiriki atamani kushiriki kila mwaka. Baadhi wameshiriki katika matembezi hayo mara kadhaa na bado wanatamani kufanya safari hiyo kila mwaka.

Matembezi hayo ni uthibitisho wa ahadi ya kushikilia misingi aliyopigania Imam Hussein (AS) na yanonyesha sura halisi ya Uislamu, ambayo ni wema na umoja bila kujali tofauti. Aidha matembezi ya Arabeen ni maandamano ya kupinga dhulma, madhalimu na  ugaidi.

A group of youth walking toward Karbala during Arbaeen procession in September 2022.

Halikadhalika matembezi ya Arabeen yanalenga kuweka hai harakati ya Karbala na kutuma ujumbe wa harakati hii kwa vizazi vijavyo. Pia yanalenga kulinda na kukuza tunu za kibinadamu za upendo na huruma na kulaani dhuluma.

Na Maryam Qarehgozlou

3480489

captcha