IQNA

Arbaeen 1435

Mtazamo wenye muono wa mbali kuhusu Arbaeen

21:04 - September 02, 2023
Habari ID: 3477537
TEHRAN (IQNA) – Mtazamo wa muono wa mbali wenye kuainisha mwelekeo kwa safari ya kidini au Ziara ya Arabeen ni muhimu sana.

Haya ni kwa mujibu wa Hujjatul Shahabeddin Doaei, mtafiti, ambaye alitoa matamshi hayo katika mkutano unaoangazia Arabeen* ya Imam Hussein AS.

Zifuatazo ni dondoo za hotuba Hujjatul Shahabeddin Doaei:

Tukilichukulia suala la siku ya Arbaeen kuwa ni suala la ustaarabu, basi tutaliangazia kwa mtazamo wa mustakabali wa ustaarabu, lakini tukilichukulia kuwa ni nembo tu ya kidini, itabaki kuwa hivyo.

Tunapaswa kuigeuza Arbaeen kuwa mazungumzo maishani na tuwe na maono bora zaidi na kuyapanga katika miaka ijayo.

Ziara ya Arbaeen sio ibada inayoanza wakati fulani mahali fulani na kuishia wakati na mahali pengine. Ina maudhui na somo tukufu.

Tunapaswa kufanya juhudi ili Arbaeen ibadilike kutoka kwenye ibada ya kibinafsi na ya kijamii na kuwa mkondo wenye ushawishi katika Uislamu na iwe kama utangulizi wa ustaarabu mpya wa Kiislamu, kwa sababu ina uwezo huo.

Arbaeen inaashiria umoja wa waumini karibu na nguzo ya Uimamu na mapenzi kwa Imam Hussein (AS). Ikiwa tunataka kujenga ustaarabu kama huo, tunapaswa kuwa na uwezo wa kuunda na kuimarisha umoja na kuwa na mwingiliano wa juu na madehebu zingine

Wakati mwanadamu ndiye mhimili wa ustaarabu wa kimaada, katika Arbaeen mhimili wake ni Uimamu. Hapa, hali ya kiroho na kumfikia Mwenyezi Mungu ndio jambo kuu ambapo kama ilivyo katika ubepari, suala kuu ni mtaji.

Ikiwa ustawi ndio lengo kuu katika ustaarabu wa Magharibi na ubinadamu hujitolea amani yake kwa ajili ya kufikia ustawi, katika Arbaeen kuna amani ambayo inatokana na shida. Yaani, watu wanakubali kupitia magumu ili kufikia jamii bora yenye msingi wa Mungu na katika mchakato huo, wanafikia pia amani na kuifurahia.

Furaha hii ni kwamba wafanyaziara au mazuwar hawaoni ugumu wowote kuwa kizuizi cha kwenda tena kwa ajili ya ziara.

Arbaeen ni fursa ya mwingiliano unaozingatia wema na ubora ili wote wafikie lengo lao. Ndio maana wengi wanatoa huduma kwa wafanyaziara kwa wema na upendo

Arbaeen ni tukio la kipekee duniani.

Bila ya serikali kuhusika, wafanyaziarai milioni 20 wanakwenda Karbala na watu wenyewe wanasimamia halaiki hii kubwa ya wageni.

Arbaeen ni tukio linaloathiri maisha na muundo wa kijamii. Hiyo ni kusema, Arabeen ina muendelezo wa kijamii ili tuweze kutekeleza malengo ya Imam Hussein (AS) katika maisha yetu.

* Inafaa kuashirikia hapa kuwa, Arbaeen ni neno la Kiarabu ambalo maana yake ni 40.  Katika muktadha huu, ni siku ya 40 tangu maadhimisho ya kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), Imam Hussein (AS) na masahaba wake watiifu tarehe 10 Muharram katika siku ya Ashura. Mtukufu huyo aliuawa shahidi katika mapambano ya Karbala  karne 14 zilizopita.

Siku ya Imam Hussein (AS) ya Arbaeen inakuja tarehe 20 Safar, mwezi wa pili wa kalenda ya mwandamo wa Kiislamu.

Baada ya kufa shahidi Imam Hussein (AS) mikononi mwa katili Yazid bin Muawiya, watu ambao walishangazwa na ukatili wa ukoo wa Ummaya walianza kuzuru kaburi lake kutoa heshima zao na tokea wakati huo hadi leo vizazi katika umma wa Kiislamu vimeendeleza utaratibu huo. Kila mwaka idadi ya wafanyaziara katika Siku ya Arabeen inaongezeka ambapo mwaka uliopita idadi hiyo ilivunja rekodi na kufika milioni 21.

Habari zinazohusiana
captcha