IQNA

Diplomasia

Mkutano wa kilele wa BRICS watoa azimio maalum kwa ajili ya kuunga mkono Palestina

17:03 - August 25, 2023
Habari ID: 3477497
TEHRAN (IQNA)-Mkutano wa kilele wa BRICS ulitoa wito wa kuanzishwa kwa taifa huru la Palestina na Jerusalem Mashariki kama mji mkuu wake.

Jumuiya ya BRICS inayojumuisha Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini ilitoa azimio kufuatia mkutano wake uliofanyika Alhamisi nchini Afrika Kusini, Pretoria, ikitaka kutekelezwa maazimio ya Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na suala la Palestina likiwemo Azimio nambari 2334 kuhusu suluhu la mzozo wa Palestina na Israel ndani ya mfumo wa suluhu ya mataifa mawili, kwa kuanzisha taifa la Palestina na Al Quds (Jerusalem) Mashariki kama mji mkuu wake.

Ujumbe kutoka Chama cha Ukombozi wa Palestina (PLO), unaoongozwa na Azzam Al-Ahmad, na mwanadiplomasia mwandamizi wa Palestina Salman Al-Harfi walihudhuria kikao cha jana.

Kando ya mkutano huo, wajumbe walikutana na idadi kadhaa ya Chama cha African National Congress (ANC) na Chama cha Kikomunisti, na kujadili maendeleo ya hivi karibuni katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Hayo yanajiri wakati ambao Muungano wa kiuchumi wa BRICS wa masoko yanayoibuka duniani umeamua kutoa mialiko ya uanachama kwa mataifa sita.

Hayo yamedokezwa Alhamisi na Rais Cyrial Ramaphosa wa Afrika Kusini ambaye ni mwenyekiti wa sasa wa BRICS.

Muungano wa BRICS - ambao kwa sasa unaundwa na Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini - unatarajiwa kuzialika Argentina, Misri, Ethiopia, Iran, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu kujiunga.  Katika hotuba iliyochapishwa kwenye X, jukwaa la mitandao ya kijamii, ambalo hapo awali liliitwa Twitter, Ramaphosa amesema BRICS ni kundi la mataifa mbalimbali.

4164742

captcha