IQNA

Watetezi wa Qur'ani Tukufu

Nchi za Kiislamu kukutana kujadili kuvunjiwa heshima tena Qur'ani barani Ulaya

20:52 - July 23, 2023
Habari ID: 3477328
BAGHDAD (IQNA)- Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq imetangaza kuwa, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) inapanga kufanya kikao cha dharura ili kujadili vitendo vya mara kwa mara vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu barani Ulaya.

Wizara hiyo imeeleza katika taarifa kwamba mkutano wa mawaziri wa OIC unatazamiwa kuitishwa kufuatia matukio ya hivi majuzi yanayohusu kutusiwa na kuvunjiwa heshima kitabu kitakatifu cha Waislamu cha Qur'ani katika nchi za Uswidi na Denmark.

Hata hivyo, taarifa hiyo haijabainisha muda na mahali utakapofanyika mkutano huo wa dharura wa OIC. Kwa mujibu wa shirika la habari la Iraq (INA), taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje imefafanua kuwa, mkutano huo utafanyika kujibu maombi mawili yaliyowasilishwa na wizara hiyo kwa OIC kuhusu matukio yaliyojiri Uswidi na Denmark, ambayo yametonesha hisia za Waislamu wapatao bilioni mbili duniani.

Taarifa hiyo imeendelea kubainisha kuwa mkutano huo wa dharura unatarajiwa kuandaa "taratibu muhimu zaidi za pamoja na misimamo ya nchi wanachama" kuhusu kesi za hivi karibuni za kutusiwa na kuvunjiwa heshima kitabu kitukufu cha Waislamu cha Qur'ani na  kupanga pia "taratibu za kukabiliana na uenezaji chuki dhidi ya Uislamu."

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq imefafanua katika taarifa yake kwamba, vitendo vya kichochezi na vya kuchukiza dhidi ya matakatifu ya Kiislamu vinachochewa na sheria zinazoviruhusu kwa kisingizio cha uhuru wa kutoa maoni na haki ya kuandamana, hatua ambayo inafufua chuki na misimamo mikali na ya kufurutu mpaka, inatishia amani na usalama wa kijamii, na kurudisha jamii za wanadamu kwenye zama za vurugu."

Baada ya raia mmoja wa Uswidi kuivunjia heshima tena Qur'ani Tukufu mbele ya ubalozi wa Iraq mjini Stockholm Alkhamisi iliyopita, genge jingine la mrengo wa kulia lenye misimamo mikali limemuunga mkono mtenda jinai huyo kwa kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu mbele ya ubalozi wa Iraq mjini Copenhagen, Denmark.

3484456

 

Habari zinazohusiana
Kishikizo: uswidi oic qurani tukufu
captcha