IQNA

Chuki dhidi ya Uislamu

EU yatetea uhuru wa kujieleza sambamba na kulaani kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini Uswidi

10:27 - July 02, 2023
Habari ID: 3477225
BRUSSELS (IQNA)- Umoja wa Ulaya umelaani vikali tukio la hivi majuzi la kuchomwa moto nakala ya Qur'ani Tukufu nje ya msikiti katika mji mkuu wa Stockholm nchini Uswidi, na kulitaja kuwa ni "kitendo cha wazi cha uchochezi."

Katika taarifa siku ya Jumamosi, EU ilisema kitendo hiki cha "kuudhi, kisicho na heshima" hakiakisi maoni ya umoja huo, ikisisitiza kwamba "dhahiri za ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya wageni, na kutovumiliana" hazina nafasi barani Ulaya.

Iliendelea kusema kwamba EU inaendelea kushikilia uhuru wa dini au imani na uhuru wa kujieleza, ndani ya nchi wanachama na kimataifa.

Taarifa hiyo ilisisitiza zaidi kwamba “sasa ni wakati wa kusimama pamoja kwa ajili ya kuelewana na kuheshimiana na kuzuia ongezeko lolote zaidi.”

Pia ilibainisha kuwa tukio hilo lilionekana kuwa la kuudhi zaidi kwani lilitokea wakati Waislamu walipokuwa wakisherehekea siku kuu ya Eid Al-Adha.

Siku ya Jumatano, mwanamume mwenye umri wa miaka 37 mwenye asili ya Iraq aliikanyaga Qur'ani Tukufu kabla ya kutekteza moto kurasa kadhaa za Kitabu hichi Kitukufu mbele ya msikiti mkubwa kabisa wa Stockholm. Kitendo hicho cha kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu kiliifanywa chini ya idhini na ulinzi wa polisi wa Uswidi.

Tukio hilo lililosadifiana na kuanza kwa siku kuu ya Eid al-Adha ya Waislamu inayoashiria kumalizika kwa ibada ya kila mwaka ya Hija mjini Makka nchini Saudi Arabia, liliibua hasira za Waislamu kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Siku ya Ijumaa, maelfu ya Wairaq walikusanyika karibu na ubalozi wa Uswidi katika mji mkuu wa Iraq wa Baghdad kwa siku ya pili ya maandamano ya kupinga kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu.

Waislamu katika nchi nyingine za Kiislamu pia waliingia mitaani kupinga hatua hiyo.

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imeitisha kikao cha dharura cha kamati yake ya utendaji kujadili hatua za kukabiliana na kitendo hicho cha kufuru.

Uswidi imeruhusu mara kwa mara kuchomwa kwa Qur'ani Tukufu katika miaka ya hivi karibuni. Mwezi Januari, mwanasiasa mwenye msimamo mkali kutoka Uswidi na Denmark alichoma nakala ya Qur'ani karibu na ubalozi wa Uturuki mjini Stockholm.

3484159

Habari zinazohusiana
Kishikizo: uswidi qurani tukufu
captcha