IQNA

Chuki dhidi ya Uislamu

Baraza la Haki za Kibinadamu la UN kujadili tukio la kuchomwa moto Qur'ani nchini Uswidi

19:09 - July 04, 2023
Habari ID: 3477236
Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa litafanya mkutano wa dharura kwa ombi la Pakistan kufuatia kuchomwa moto Qur'ani nje ya msikiti mmoja nchini Uswidi au Sweden.

Hayo yameelezwa na semaji wa baraza hilo la Umoja wa Mataifa lenye makao yake makuu mjini Geneva katika mkutano aliofanya na waandishi wa habari leo na kuongeza kuwa majadiliano yatafanyika baadaye wiki hii katika baraza la haki za binadamu kuhusiana na kuongezeka kwa chuki za kidini.

Kitendo cha kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu kilifanywa wiki iliyopita na mtu mmoja nje ya msikiti mkuu wa mji mkuu wa Uswidi, Stockholm wakati wa maandamano yaliyoidhinishwa na polisi ya nchi hiyo.

Serikali ya Uswidi imetoa tamko la kulaani kitendo hicho cha "uenezaji chuki dhidi ya Uislamu", baada ya chombo cha kimataifa cha Kiislamu cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC kutaka zichukuliwe hatua kuepusha kuvunjiwa heshima kitabu hicho kitakatifu cha Waislamu katika siku za usoni.

Viongozi wa nchi kadhaa, zikiwemo nyingi za Magharibi ya Asia, wamekemea na kulaani tukio hilo na kuitaka Stockholm ichukue hatua zaidi dhidi ya chuki za kidini.

Mbali na kulaani, Morocco ilikwenda mbali zaidi kwa kumrudisha nyumbani balozi wake nchini Uswidi kwa muda usiojulikana.

Wakati huo huo, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema: "tutawafundisha watu wa Magharibi wenye kiburi kwamba sio uhuru wa kujieleza kutusi maadili matakatifu ya Waislamu."

Kwa upande wa viongozi wa kidini, Mufti wa Oman Sheikh Ahmad bin Hamad al Khalili amewatolea wito Waislamu duniani kote kususia bidhaa za Uswidi na kuzitaka taasisi na jumuiya zote za Kiislamu zikiwemo serikali za nchi kufutilia mbali ushirikiano wa kibiashara na kifedha na nchi hiyo.

/3484209

Habari zinazohusiana
Kishikizo: uswidi qurani tukufu
captcha