IQNA

Watetezi wa Qur'ani Tukufu

Watu wa Bangladesh waandamana kulaani kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu

15:16 - August 08, 2023
Habari ID: 3477397
TEHRAN (IQNA) – Maandamano makali yalifanyika nchini Bangladesh baada ya makumi ya nakala za Qur’ani Tukufu kuchomwa moto katika nchi hiyo ya Kusini mwa Asia.

Polisi walisema walifyatua risasi za mpira na vitoa machozi kutawanya umati wa "angalau watu 10,000" usiku kucha kuanzia Jumapili hadi Jumatatu walipokuwa wakijaribu kuwashambulia watu hao wawili wanaotuhumiwa kwa kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu. Polisi kumi na wanne walijeruhiwa katika mapigano hayo.

Wanaume hao wawili walikamatwa katika mji wa kaskazini-mashariki wa Sylhet na walisema walikuwa wamechoma nakala za Qur'ani Tukufu kwa vile "zilikuwa za zamani sana na zingine zilikuwa na makosa ya uchapishaji".

Polisi waliwataja washtakiwa hao kuwa ni mwalimu mkuu wa shule Nurur Rahman na Mahbub Alam, wakisema "wamekamata nakala 45 za Qur'ani Tukufu zilizokuwa zimechomwa".

Kwa mujibu wa baadhi ya wanachuoni, kutupa nakala ya Qur'ani Tukufu ambayo haitumiki tena inajuzu iwapo jambo hilo litafanywa kwa taratibu maalumu na kwa heshima.

Mwezi uliopita mvutano ulipamba moto kati ya nchi za Kiislamu na Uswidi na Denmark kufuatia maandamano kadhaa yaliyohusisha kudhalilisha hadharani Qur'ani Tukufu - ikiwa ni pamoja na kuchoma kurasa.

Nchi zote mbili zimeshutumu kunajisi, lakini zimeshikilia sheria zao kuhusu uhuru wa kusema na kukusanyika.

Bangladesh ina wakazi milioni 170, asilimia 90 kati yao ni Waislamu.

 

Habari zinazohusiana
captcha