IQNA

Watetezi wa Qur'ani Tukufu

Kuvunjia heshima Qur’ani Tukufu hueneza ubaguzi, chuki

20:43 - August 28, 2023
Habari ID: 3477509
BAGHDAD (IQNA) - Washiriki katika kongamano la kimataifa lililofanyika kwa njia ya intaneti kujadili suala la kuvunjiwa heshima Qur'ani hivi karibuni barani Ulaya walisisitiza kwamba vitendo hivyo viovu vinakiuka haki za kimsingi mbali na kueneza chuki na ubaguzi.

Kongamano la mtandanoni la  "Dhamira ya Vyuo Vikuu vya Ulimwengu wa Kiislamu katika Kukabiliana na Kuvunjiwa heshima kwa Qur'ani Tukufu na Seerah Nabawi" liliandaliwa kwa pamoja Jumapili na Chuo Kikuu cha Isfahan cha Iran na Chuo Kikuu cha Imam Kadhim (AS) cha Iraq.

Noufel Rahman al-Jabouri, naibu Kansela wa Chuo Kikuu cha Imam Kadhim (AS) alisema katika semina hiyo ya mtandaoni kwamba, uchomaji moto wa hivi karibuni wa Qur'ani Tukufu ni matokeo ya kushindwa moja kwa moja na kwa njia isiyo ya moja kwa moja kukabiliana na vitendo vya kuvunjia heshima matukufu ya kidini.

Alisisitiza haja ya kuongeza mwamko katika jamii kusimama dhidi ya vitendo hivyo viovu , na kuongeza kwamba kuna ulazima wa kuheshimu imani za wengine, kuwa na uvumilivu, na kuishi pamoja kwa amani miongoni mwa wafuasi wa imani tofauti unapaswa kukuzwa.

Al-Jabouri pia ametaka hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wale wanaovunjia heshima Waislamu na matukufu ya Kiislamu.

Ameongeza kuwa, kuichoma moto na kuivunjia heshima Qur’ani  Tukufu ni ukiukaji wa haki za kimsingi za Waislamu na kueneza mbegu za ubaguzi na chuki baina ya watu.

Aqil Jassim Kadhim al-Muhammadawi, mkurugenzi wa idara ya Qur'ani na Hadith ya Chuo Kikuu hicho, alikuwa mzungumzaji mwingine katika mtandao huo.

Alikosoa kukosekana hatua za kivitendo za  baadhi ya viongozi na wanazuoni wa vyuo vikuu katika kukabiliana na kuvunjia heshima Qur’ani Tukufu.

Vile vile ametoa wito kwa wanafunzi wa Kiislamu kujizatiti na mafundisho ya Quran ili kukabiliana na mawazo potofu.

Al-Muhammadawi pia alisisitiza haja ya kutengenezwa vituo vya Qur'ani na kusaidia miradi na programu za Qur'ani.

Profesa wa Chuo Kikuu cha Isfahan, Mohammad Reza Sotudehnia pia alihutubia mtandao huo, akisisitiza kwamba majaribio ya kuchafua Qur'ani yatashindwa kudhoofisha hadhi tukufu ya Kitabu hicho Kitukufu.

Amesema ni lazima wasomi wa vyuo vikuu na shakhsia waungane dhidi ya maadui wa Qur’ani Tukufu.

Aidha ametoa wito wa kuanzishwa kituo cha ufuatiliaji wa masuala yanayohusiana na Qur'ani Tukufu duniani.

Katika wiki za hivi karibuni, kudhalilishwa kwa Qur'ani Tukufu nchini Uswidi, Denmark na Uholanzi kwa idhini ya serikali na ulinzi wa polisi kumezua hasira na shutuma nyingi kutoka kwa ulimwengu wa Kiislamu.

Nchi za Ulaya zinaruhusu vitendo vya kuvunjia heshima Qur’ani Tukufu chini ya kivuli cha kile kinachoitwa uhuru wa kujieleza licha ya kulaaniwa na mataifa ya Kiislamu na yasiyo ya Kiislamu na hata mbele ya azimio la Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa.

3484950

Habari zinazohusiana
Kishikizo: watetezi wa qurani
captcha