IQNA

Watetezi wa Qur'ani Tukufu

Waislamu duniani kote waungana kupinga kuvunjiwa heshima Qur'ani barani Ulaya

18:50 - July 24, 2023
Habari ID: 3477329
TEHRAN (IQNA)- Waislamu katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo Iran, Iraq, Lebanon na Nigeria wamefanya maandamano makubwa na kulaani kitendo cha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini Sweden.

Katika siku 10 za karibuni vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu vimeshika kasi zaidi katika nchi za Ulaya. Uswidi na Denmark, kwa mara nyngine tena, zimetoa kibali cha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika nchi hizo. Kwa mara ya pili katika muda wa wiki moja, Alhamisi iliyopita wahalifu wa Uswidi waliivunjia heshima Qur'ani Tukufu kwa kutumia kibali walichopewa na polisi wa nchi hiyo. Juzi Ijumaa pia kundi moja lenye misimamo ya kufuruti ada huko Denmark lilichoma moto nakala ya Qur'ani mbele ya ubalozi wa Iraq huko Copenhagen mji mkuu wa nchi hiyo.  

Kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu huko Uswidi na Denmark kunaonyesha kuwa, licha ya serikali za nchi za Ulaya kudai kwamba haziungi mkono kudhalilishwa Qur'ani katika sera zao, lakini kivitendo nchi hizo zinaunga mkono na kuhamasisha vitendo hivyo vilivyo kinyume na sheria na vya kijahili.

Mtazamo wa serikali za Ulaya

Serikali za nchi za Ulaya licha na kushuhudia namna Waislamu, katika nchi mbalimbali, walivyokasirishwa na kughadhibishwa na hujuma hizo lakini zinaandaa mazingira ya kuendelezwa vitendo hivyo badala ya kukabiliana na uhalifu huo dhidi ya matukufu ya kidini ya Waislamu zaidi ya bilioni mbili. Nchi hizo zinahalalisha vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu kwa madai ya uhuru wa kujieleza, lakini wakati huo huo zinawazuia wanafunzi wa kile Waislamu kuvaa vazi la stara la hijabu mashuleni au kuhoji na kudadisi tu madai ya Holocaust. Katika mazingira na hali kama hii, uhuru wa kujieleza huwa hauna maana yoyote. Kwa msingi huo, kuyavunjia heshima na kutangaza chuki dhidi ya matukufu ya Kiislamu katika nchi za Ulaya si uhuru wa kusema na kujieleza, bali ni hatua iliyokusudiwa na inayofanyika kwa mpangilio maalumu dhidi ya dini ya Uislamu na Waislamu.

Hatua hii ya serikali za nchi za Ulaya na wajinga wanaoivunjia heshima Qur'ani Tukufu imekabiliwa na msimamo mkali wa Waislamu kote duniani.

Anayevunjia heshima Qur'ani tukufu aadhibiwe

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kutovukiwa adabu matukufu ya Waislamu hasa Qur'ani Tukufu huko nchini Uswidi ni tukio chungu na ni njama hatari sana akisisitiza kuwa, aliyefanya jinai hiyo lazima aadhibiwe, na maulamaa wote wa Kiislamu wanaafikiana katika hilo.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo katika ujumbe maalumu wa maandishi na kuongeza kuwa, serikali ya Uswidi na wajibu wa kumtia mbaroni aliyefanya jinai hiyo na kumkabidhi kwa idara za mahakama za nchi za Waislamu. 

Sehemu moja ya ujumbe huo muhimu wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu inasema: Serikali ya Uswidi inapaswa kuelewa kwamba, hatua yake ya kuunga mkono vitendo vya jinai imeifanya itangaze vita na Ulimwengu wa Kiislamu na ijipalilie chuki na uadui kutoka kwa kila Muislamu na serikali nyingi za Waislamu duniani. 

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa, jukumu la serikali ya Uswidi ni kumtia mbaroni aliyetenda jinai hiyo na kumkabidhi kwa mahakama za nchi za Waislamu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesisitiza kuwa, wanaofanya njama hizo nyuma ya pazia nao wanapaswa kuelewa kuwa, Qur'ani Tukufu inaendelea kunawiri siku baada ya siku na nuru yake itazidi kung'ara na kwamba njama na vitendo kama hivyo ni dhalili mno kuweza kuzuia kuenea nuru ya Qur'ani kwenye nyoyo za walimwengu.

Msimamo imara wa serikali ya Iraq

Baada ya kuuvamia ubalozi wa Uswidi, waandamanaji waliokuwa na hasira huko Iraq wameushambulia pia ubalozi wa Denmark mjini Baghdad wakipinga uhalifu huo. Wanadiplomasia na wafanyakazi wa ubalozi wa Uswidi tayari wamefukuzwa nchini Iraq. Wakati huo huo Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq imeitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za kuzuia kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu na kukikaja kitendo hicho kuwa ni kiovu na cha kuchukiza. 

Huko Lebanon na Nigeria pia wananchi wameandamana kupinga vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu na kutaka kufukuzwa balozi wa Uswidi katika nchi hizo. Miji mbalimbali ya Iran pia juzi Ijumaa ilishuhudia maandamano makubwa ya kulaani na kupinga kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu. Waandamananaji hao wamesisitiza kuwa, kuna ulazima wa kukabiliana na nchi zinazoruhusu vitendo hivyo vya udhalilishaji dhidi ya kitabu kitakatifu cha Waislamu.

Katika mkondo huo, Hossein Amir- Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia ametangaza kuwa: "Tehran haitampokea balozi mpya wa Uswidi, na balozi mpya wa Iran hatatumwa huko Uswidi." Amir- Abdollahian pia ametaka kuitishwa kikao cha dharura cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kujadili kadhia ya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika nchi za Ulaya. Saudi Arabia, Imarati na Jordan pia zimewaita mabalozi wa Uswidi kwa ajili ya kujieleza.

Wakati huo huo  vyombo vya habari vya Lebanon vimetoa wito wa kufukuzwa balozi wa Uswidi nchini humo. Uturuki kwa upande wake imetoa hukumu ya kukamatwa watu wanaoivunjia heshima Qur'ani Tukufu. 

Uwezo mkubwa wa Waislamu

Bila shaka, waliopata hasara kubwa katika makabiliano na Uislamu katika nchi za Ulaya ni serikali za Ulaya na Umoja wa Mataifa. Ulimwengu wa Kiislamu una suhula na uwezo mkubwa katika nyanja mbalimbali hususan katika sekta ya kiuchumi; ambapo kuongezeka pengo kati ya nchi za Kiislamu na zile za Ulaya kutazizuia nchi hizo kunufaika na suhula hizo za nchi za Kiislamu. 

Katika upande mwingine, Umoja wa Mataifa ambao aghalabu ya hati nyaraka zinazohusiana na haki za kimataifa zimepasishwa kwa usimamizi wake, haujachukua msimamo imara wa kukabiliana na vitendo vichafu vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu; kwa msingi huo nafasi ya Umoja wa Mataifa na hati hizo zitatiliwa shaka na kupoteza hadhi na heshima kutokana na msimamo wake dhaifu kuhusu suala hili.

3484475

Habari zinazohusiana
Kishikizo: uswidi qurani tukufu
captcha