IQNA

Uchambuzi

Kuendelea kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu na ulazima wa nchi za Kiislamu kutoa jibu kali

21:54 - July 22, 2023
Habari ID: 3477322
TEHRAN (IQNA) Kwa mara ya pili katika kipindi cha wiki kadhaa za karibuni, wahusika wa kuchoma moto Qur'ani Tukufu huko Uswidei wamekivunjia heshima kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu kwa ruhusa ya polisi ya nchi hiyo na baada ya kupewa kibali cha kuandamana dhidi ya Uislamu katika mji mkuu wa nchi hiyo, Stockholm.

Aidha kundi la watu wenye itikadi kali dhidi ya Uislamu lilifanya kitendo cha uchochezi cha kuvunjia heshima Qur'ani katika mji mkuu wa Denmark Copenhagen siku ya Ijumaa, na kuzusha hasira miongoni mwa Waislamu waliozitaka mamlaka kuzuia vitendo hivyo vya chuki kurudiwa.

Katika kadhia ya Uswidi, Salwan Momika raia wa Uswidi mwenye asili ya Iraq kwa mara nyingine tena ameivunjia heshima Qur'ani Tukufu huku akilindwa na polisi wa katika nchi hiyo ya Skandinavia na kisha akaichoma moto bendera ya Iraq.

Polisi ya Uswidi siku kadhaa kabla ya hujuma hii tajwa walitangaza kuwa wametoa kibali cha kufanyika maandamano ya upinzani nje ya ubalozi wa Iraq huko Stockholm. Awali, baadhi ya vyombo vya habari viliripoti kuwa watu walioitisha maandamano hayo walikuwa na lengo la kuchoma moto tena kitabu hicho kitukukfu cha Waislamu. 

Waislamu wamekasirishwa  

Tukio hili limewakasirisha pakubwa Waislamu duniani na hasa Waislamu wa Iraq; na kuwapelekea wakazi wa mji mkuu Baghdad kuandamana na kukusanyika katika mitaa ya pambizoni mwa ubalozi wa Usiwdi mjini humo ambapo wameshambulia milango mikuu ya kuingia katika ubalozi huo na kuchoma moto baadhi ya maeneo ya jengo la ubalozi. Hali hii ya mambo imeibua mivutano ya kidiplomasia kati ya nchi mbili za Iraq na Sweden; ambapo serikali ya Iraq imechukua uamuzi wa kumtimua nchini humo Balozi wa  Uswidi. Ofisi ya Waziri Mkuu wa Iraq awali ilikuwa imeitahadharisha Stockholm kwamba itakata uhusiano na Uswidi iwapo kitendo cha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu kitakaririwa tena.

Kuenea chuki dhidi ya Uislamu

Chuki dhidi ya Uislamu na vitendo vya mabavu dhidi ya Waislamu vimeongezeka sana katika miaka ya karibuni katika nchi za Ulaya. Wakati huo huo kudhihiri pakubwa harakati na vyama vya mrengo wa kulia vyenye misimamo mikali, na pia hatua ya serikali za Magharibi ya kuanzisha anga ya propaganda dhidi ya Waislamu imezifanya nchi za Ulaya zinazodai eti kuheshimu uhuru wa kujieleza kutoa fursa kwa wale wote wanaoyadhalilisha na kuyavunjia heshima matukufu ya zaidi ya watu bilioni moja na nusu duniani kote. Hii ni katika hali ambayo, huko nyuma Miguel Moratinos, Mwakilishi Mkuu wa Muungano wa Tamaduni wa Umoja wa Mataifa alisistiza umuhimu wa kulindwa uhuru wa kujieleza kama haki ya msingi ya mwanaadamu; na wakati huo huo akatahadharisha kuwa kukidhalilisha Kitabu Kitukufu na maeneo ya kufanyia ibada na pia nembo za kidini ni jambo lisilokubalika na linaweza kuchochea machafuko." 

Mtazamo wa undumakuwili wa nchi za Magharibi kuhusiana na suala zima la uhuru unaonyesha kuwa suala hilo hilo hupewa umuhimu pale tu linapohusu chuki dhidi ya Uislamu na kutusi matukufu ya Waislamu na wala serikali za Ulaya huwa jazifafanui maana halisi ya neno uhuru. Kama ilivyokuwa katika kadhia ya Holocaust, zilitoa radiamali kali kwa wale wote waliodhihirisha msimamo unaokinzana katika uwanja huo kinyume na mitazamo yao na hata kuchukua hatua ya kuwafunga jela watuhumiwa.   

Mtazamo wa Kanisa Katoliki

Papa Francis Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani anazungumzia hili kwa kusema: Uhuru wa kujieleza kamwe haupasi kutumiwa kama kisingizio cha kuchochea wengine; na kuruhusu  vitendo kama kuchoma moto Kitabu cha Mwenyezi Mungu ni hatua inayopasa kulaaniwa." 

Nchi za Kiislamu zichukue hatua

Kukaririwa udhalilidhaji huu dhidi ya Qur'ani Tukufu kunaonyesha namna nchi za Magharibi zisivyo na aibu katika kuwavunjia heshima Waislamu na imani zao huku zikifuatilia sera za chuki dhidi ya Uislamu kwa sura tofauti. Kwa msingi huo, inaonekana kuwa nchi za Kiislamu zinapasa kuchukua msimamo mkali zaidi na wa pamoja na hasa taasisi kama Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu (OIC), Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) n.k, ambapo sambamba na kulaani kitendo hiki, zichukue hatua za kivitendo za kupambana na siasa hizo. Wakati huo huo, kukata uhusiano wa kisiasa na kibiashara kati ya nchi za Kiislamu na Uswidi au kususia bidhaa za nchi hiyo pia inaweza kuwa sehemu ya kampeni kubwa ya Waislamu ya kupinga hatua ya serikali ya Uswidi ya kutoa kibali cha kuchomwa moto Qur'ani Tukufu nchini humo. 

4156938

Habari zinazohusiana
Kishikizo: uswidi qurani tukufu
captcha