IQNA

Watetetezi wa Qur'ani Tukufu

Wananchi wa Yemen wafanya Mkutano Mkubwa Sana’a kulaani Matukio ya Kuvunjia heshima Qur'ani

20:12 - July 26, 2023
Habari ID: 3477346
SANAA (IQNA) - Maandamano makubwa yalifanyika Sana'a, mji mkuu wa Yemen, kulaani unajisi wa hivi majuzi wa maeneo matakatifu ya Kiislamu nchini Uswidi na Denmark.

Uwanja wa Bab Al-Yemen huko Sana'a ulishuhudia maandamano hayo makubwa Jumatatu alasiri. Washiriki hao wamelaani jinai ya kuchoma Qur'ani Tukufu nchini Uswidi na Denmark.

Maandamano hayo ya hasira yalianza kwa kukariri aya za Qur'ani Tukufu, na kufuatiwa na washiriki wakipiga nara dhidi ya maadui wa Uislamu na Waislamu. Katika hafla hiyo, washiriki walisisitiza kuwa, kuchomwa moto Qur'ani na nchi potovu ni ushahidi wa jinai zao, utegemezi wao kwa lobi ya Wazayuni, na kujisalimisha kwao kwa Marekani na utawala wa Kizayuni. "Tulitoka leo kusema kwamba nyuma ya Quran ni taifa la Quran. Kuchoma Quran ni kufichuliwa kwa maadui wa taifa na mazingira mapya ya dira kuelekea maadui wa Quran," alisema muandamanaji. Waandamanaji walionyesha azma ya Yemen ya kususia bidhaa zinazotengenezwa na Uswidi, Denmark, na nchi yoyote inayoshambulia Kitabu cha Mwenyezi Mungu.

Baraza la Mawaziri la Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen limetoa wito kwa nchi za Kiislamu kuchukua hatua za kivitendo ili kukabiliana na mashambulizi dhidi ya matukufu ya Kiislamu.

Taarifa iliyotolewa na Baraza la Mawaziri la Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen imetoa wito wa kusitishwa uhusiano wa kidiplomasia na Uswidi na nchi nyingine za Ulaya zinazokashifu na kuvunjia heshima dini ya Kiislamu.

Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen pia imesisitiza udharura wa kutekelezwa ipasavyo azimio la vikwazo na kususia bidhaa za Sweden na nchi nyingine zinazokashifu kwa makusudi nembo na matukufu ya Kiislamu.

Taarifa ya Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen pia umepongeza hatua ya serikali ya Iraq ya kukata uhusiano wa kidiplomasia na Uswidi na kumfukuza balozi wa nchi hiyo mjini Baghdad.

Awali Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Serikali ya Uokoaji wa Kitaifa ya Yemen ilitangaza kuwa, kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu ni matokeo ya chuki dhidi ya Uislamu barani Ulaya.

3484497

Habari zinazohusiana
Kishikizo: uswidi qurani tukufu
captcha